Kuna kijiji kimoja kulikuwa na mama mmoja kichaa, yule mama akawa anapita mitaani na kupiga kelele huku akisema "Ukitenda mema unajitendea mwenyewe na ukitenda mabaya, unajitendea mwenyewe"

Basi kila siku alikuwa anazunguka na kusema maneno hayo hayo, akisikia njaa anaenda nyumba yoyote anaomba chakula anakula anaendelea na safari zake kama kawaida

Kutokana na hilo, akawa amezoeana na watoto wote wa kile kijiji, siku moja mama mmoja akasema "Huyu kichaa anasumbua sana na anaharibu watoto wetu tumuuwe"

Siku iliyofuata yule kichaa na kelele zake kama kawaida akafika kwenye ile nyumba ya yule mama akaomba chakula, yule mama akachukua mikate akaweka sumu akampa, yule kichaa akaondoka zake na mikate yake mkononi, njiani akakutana na watoto wanatoka shuleni, wakaanza kumchezea kama kawaida yao yeye akawapa ile mikate wakala

Baada ya kuwapa mikate yeye akaendelea na safari zake, watoto walipofika nyumbani, wakaanza kuumwa matumbo mama yao akawauliza "Mmekula nini shuleni?" wakamjibu "Hatujala chochote ila tulikutana na 'Ukitenda Mema , Umejitendea Mwenyewe' akatupa mikate tukala", yule mama akaweka mikono kichwani akaanguka na kupoteza fahamu

Baada ya kuzinduka akakuta watoto wake wote wamepoteza maisha

UKITENDA MEMA, UNAJITENDEA MWENYEWE na UKITENDA MABAYA UNAJITENDEA MWENYEWE

#ChekanaZephiline