Tukio la Kweli Katika Maisha Halisi(Dan Cooper) 7c582e10
Siku ya November 24 mwaka 1971, katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mji wa Portland jamaa aliyevaa suti nyeusi na koti refu jeusi kwa juu akiwa amebeba brief case nyeusi alifika katika counter ya kampuni ya ndege ya Northwest Orient Airlines na akatoa fedha cash dola 20 kununua tiketi ya ndege Flight 305 kwenda mjini Seattle, ambayo kwa kawaida ni safari inayochukua dakika 30. Jamaa huyu alijitambulisha kama 'Dan Cooper'.

Baada ya kuingia kwenye ndege akakaa kwenye siti namba 18C, baadae akakaa siti namba 18E na baadae 15D.
Ilipofika mida ya saa nane na dakika hamsini mchana ndege ikaruka na baada ya ndege kuruka Mr. Cooper akawasha sigara na akaagiza soda!
Siti ambayo alikaa Cooper ilikuwa siti ya nyuma kabisa na alikaa karibu kabisa na siti ya muhudumu wa ndege wa kike aliyeitwa Florence Schaffner.

Baada ya dakika chache Cooper alitoa kikaratasi mfukoni kilichochapwa kwa unadhifu na maandishi yakiwa yameandikwa kwa herufi kubwa na kisha akampatia Bi. Schaffner kikaratasi hicho.
Baada ya Bi. Schaffner kupokea kikaratasi, kutokana na mazoea akajua ni kawaida tu abiria alikuwa ametokea kumtamani na hivyo amempa namba ya simu, kwa hiyo Bi. Schaffner hakukisoma kikaratasi bali alikiweka moja kwa moja kwenye mkoba. Mara baada ya kukiweka kikaratasi kwenye mkoba, Cooper akainama kidogo na kumnong'oneza Bi. Schaffner na kumwambia "Miss you would better take a look at that note. I have a bomb" (Bibie ni vyema ungekisoma hicho kikaratasi. Nina bomu).

Baada ya kumueleza hivyo kimya kimya akamuamuru muhudumu huyo akae karibu nae na kuanza kumpa maagizo. Lakini kabla ya hapo yule mhudumu akataka ampe uhakika kama kweli ana bomu. Cooper akachukua briefcase yake na kuifungua kidogo tu ili muhudumu aangalie na alipoangalia ndani ya briefcase akaona cylinders nane, nne zikiwa chini na nne zikiwa juu zikiwa zimeunganishwa kwa nyaya nyekundu ambazo nazo zinaenda kuunganika kwenye battery yenye rangi nyekundu pia ikiyopo pembezoni mwa briefcase. Baada ya kuchungulia muhudumu akaamini kweli Cooper alikuwa na Bomu.

Cooper akampa maagizo muhudumu akaongee na marubani kwa kupitia intercom kuwa wawasiliane na uwanja wa ndege wa Seattle na wawaeleze juu ya ndege kutekwa na mtu mwenye bomu na yuko tayari kulipua ndege hiyo na abiria wote 36 na watumishi wa ndege 6 waliopo umo ndani.. (Ndege ilikuwa haijajaa yote, ilijaa kama theluthi moja tu (1/3)).
Ili asilipue ndege hiyo Cooper alihitaji apewe 'Fedha halali za kimarekani' dola 200,000 (msemo huu 'fedha halali za kimarekani' utakuja kuleta maana sana huko mbele kwenye upelelzi wa FBI). Pia aliamuru apewe parashuti nne na ndege itakapofika uwanja wa ndege wa Seattle kuwe na gari ya kujaza mafuta inasubiri ili ijaze ndege mafuta na kumpeleka sehemu atayoitaka.
Muhudumu Bi. Schaffner akawasiliana na mapilot na kuwahakikishia kuwa ni kweli jamaa ana bomu na akawapa orodha ya vitu alivyokuwa anavitaka.

Baada ya kupewa orodha ya demands za Bwana Cooper, marubani wakawasiliana na uwanja wa ndege wa Seattle na watu wa uwanja wa ndege wakawasiliana na vyombo vya ulinzi na baada ya mtiririko wa mawasiliano kati ya uwanja wa ndege, wamiliki wa ndege na vyombo vya ulinzi kufanyika wakakubaliana kuwa ili kuepusha hasara ya kibiashara na kupoteza maisha ya watu 42 ni vyema wakampatia mtekaji anavyovitaka lakini vyombo vya ulinzi vitaangalia kama kutapatikana fursa yoyote waweze kumkamata au kumdungua mtekaji huyo.
Hivyo basi wahudumu wote waliopo kwenye ndege waliamuliwa wampe ushiriakiano Cooper ili kuepusha hatari yoyote na pia wamueleze kuwa awape mda kidogo ili kukamilisha kupata vitu alivyokuwa anavihitaji.

Baada ya jibu hilo kurudishwa juu kwenye ndege na marubani kuwasiliana na muhudumu Schaffner kupitia intercom, muhudumu alirudi kwenye siti aliyokaa Cooper na alikuta sasa amevaa miwani meusi ya jua na yuko amerelax kabisa bila presha wala wasiwasi wowote! Akampatia jibu walilopewa kutoka chini kwenye uwanja wa ndege.
Baada ya kupewa jibu hilo Cooper akaitikia kwa kichwa kisha akawasha sigara nyingine na kuagiza Soda nyingine na maji ya kunywa, na kwa mshangao akalipia na chenji iliyorudi akampa 'tip' muhudumu Schaffner.

Muda wote huu abiria wengine walikuwa hawajui kinachoendelea ndani ya ndege na ili kuepusha wasije wakapata wasiwasi kutokana na kuchelewa kutua wakatangaziwa kuwa kulikuwa na tatizo la kiufundi hivyo itawalazimu wachelewe kutua mpaka tatizo litakapo shughulikiwa.
Kama nilivyoeleza awali kutoka Portland mpaka Seattle ni safari ya nusu saa kwa ndege lakini ndege ilikaa angani taribani masaa mawili ikiwa inazunguka tu ili kusubiria kule chini mamlaka usika ziandae vitu cooper alivyohitaji.

Ndani ya masaa mawili FBI walifanikiwa kukusanya noti za dola 20 zipatazo elfu kumi (jumla dola 200,000) kutoka bank za karibu na zote wakazipiga picha! Pia walifanikiwa kupata parashuti nne kutoka katika kituo cha jeshi la anga cha Tacoma kilichopo karibu na uwanja wa ndege wa Seattle! Baada ya kumaliza kufanya maandalizi yote haya mnamo majira ya saa kumi na moja dakika ishirini na nne wakawasiliana na ndege juu kumtaarifu Cooper kuwa vitu vyake vyote alivyohitaji viko tayari.

Baada kumpa orodha ya vitu hivyo Cooper akaamuru kuwa hataki parashuti za kijeshi anataka apewe parashuti za kawaida za kiraia na FBI wakafanikiwa kuzipata kutoka katika kituo cha kufunza watu skydiving.
Robo saa baadae (saa kumi na moja dakika 39) ndege ilitua katika uwanja wa Seattle na Cooper akamuamuru rubani aisimamishe ndege sehemu pweke na yenye mwanga wa kutosha. Pia akamuamuru rubani azime taa zote ndani ya ndege ili kuepusha wadunguaji (snipers) wa FBI kufanya yao.

Baada ya ndege kusimama mtumishi mmoja wa kampuni ya Northwest Orient Airlines aliyejulikana kama Al Lee akiwa amevalia kiraia ili kuepuka kumchanganya cooper asidhani ni askari akiwa amevaa sare za uwanja wa ndege, alikabidhiwa mabegi yaliyokuwa na fedha pamoja na maparashuti.
Al Lee akaisogelea ndege na Cooper akamuamuru muhudumu mwingine ndani ya ndege binti aliyeitwa Mucklow afungue mlango mdogo wa dharura pembeni ya ndege na kupokea mabegi hayo. Na Mucklow akatii.

Baada ya Cooper kuhakikisha kuwa fedha na kila kitu alichohitaji kiko sawa sawa akawaruhusu abiria wote washuke. Pamoja na abiria alimruhusu muhudumu Schaffner pamoja na muhudumu mwingine ambaye alikuwa anaonekana kuwa na umri mkubwa. Lakini akabaki na marubani wote wawili, yule binti mwingine muhudumu aliyeitwa Macklow pamoja na fundi wa ndege.
Kisha akaamuru gari la kujaza mafuta liletwe na kuwajazia mafuta.
Wakiwa wanawajazia mafuta Cooper aliwapa maagizo marubani kuhusu anakotaka waende na jinsi ambavyo anataka wasafiri. Kwanza akawaeleza kuwa anataka wafuate njia inayoelekea Mexico City na ndege iendeshe katika speed ya km 190/hour na ndege iruke umbali wa futi 10,000 kutoka ardhini.
Pia aliwaeleza kuwa anataka waondoe mgandamizo ndani ya ndege (cabin pressure) na wakiruka matairi yabaki kana kwamba wanatua, pia mlango wa nyuma ya ndege ubakie wazi kana kwamba mizigo inapakiwa na mabawa ya ndege ya pembeni yawekwe kwenye nyuzi 15.

Baada ya majadiliano kampuni ya Northwest Orient wakakataa ombi la cooper ndege iruke ikiwa imefunguliwa mlango wa nyuma mkiani au pembeni kwa madai kuwa itahatarisha usalama lakini Cooper kwa kujiamini kabisa akawaeleza kuwa ni salama na hakutaka kubishana nao sana kwani baada ya ndege kuruka tu aliufungua mlango wa pembeni mwenyewe.

Ndege iliruka kutoka kwenye uwanja wa ndege wa Seattle mnamo majira ya saa kumi na moja dakika arobaini ikiwa na watu watano pekee, yaani Cooper, muhudumu Macklow, fundi na marubani wawili! Watu watatu yaani fundi na marubani wawili walikuwa mbele kabisa kwenye chemba/chumba cha marubani kuendeshea ndege (cockpit) na Cooper pekee na muhudumu Macklow walokuwa kwenye sehemu ya abiria.
Mara tu baada ya ndege kuruka, ndege mbili za kivita aina ya F-106 kutoka kituo cha kijeshi cha McChord Air Force Base nazo ziliruka kuifuatilia ndege iliyotekwa na Cooper na ziliruka katika namna ambayo zisingeweza kuonekana na Cooper au mtu yeyote aliyeko ndani ya ndege, ndege moja  iliruka juu nyingine chini ya ndege ya akina Cooper.

Baada ya mda kidogo kupita Cooper ali muamuru muhudumu aende mbele kwenye chumba cha marubani na akamfungia huko pamoja na wengine na akabaki peke yake katika sehemu ya kukaa abiria.
Takribani saa mbili kamili usiku alarm ikalia mbele kwenye chumba cha marubani kuashiria kuwa kifaa cha kufungua mlango wa nyuma kwenye mkia wa ndege kimehuishwa (Deactivated). Dakika chache baadae sehemu ya nyuma ya ndege ilitikisika kwa nguvu na kuwa kama inainuliwa juu na marubaini wakabaini kuwa mlango wa nyuma kwenye mkia wa ndege ulikuwa umefunguliwa na ili kuepusha ndege isidondoke marubani iliwalazimu waishushe ndege chini na kutua kwenye uwanja wa ndege wa Reno, Nevada takribani majira ya saa nne na robo usiku.

Baada ya ndege kutua tu maofisa wa FBI na polisi waliizunguka na kuingia ndani kufanya upekuzi na ndani ya dakika chache wakagundua D.B Cooper hakuwepo ndani ya ndege.

MSAKO WA KIHISTORIA.
Tukio la Kweli Katika Maisha Halisi(Dan Cooper) 640px-10
Baada ya FBI kujiridhisha kuwa Cooper hakuwa ndani ya ndege nadharia pekee iliyobakia ni kuwa aliruka ndege ikiwa angani kwani baada ya kuipekua ndege walikuta parachuti mbili hazipo. Jambo la ajabu ni kuwa marubani wa ndege za kivita zilizokuwa zinaifuatilia ndege ya akina Cooper walisema kuwa hawakuona mtu akiruka kutoka kwenye ndege wala parachuti kufunguliwa.

Baada ya kutafakari kwa kina FBI wakaamua waitengeneza upya safari kama ile ile ambayo ilitokea siku ya tukio.
Hivyo basi kwa kutumia ndege ile ile na rubani yule yule FBI walorusha ndege kutoka uwanja wa Seattle kuelekea uwanja wa Rona, ndege ikiondoka Seattle muda unaofanana kabisa na ule ambao siku ile ya utekaji ndege iliondoka Cooper akiwemo ndani.

Kitendawili kikubwa ni mahali gani hasa ndipo kulikuwa na uwekano kuwa Cooper alitua ardhini. Lakini ili waweze kujua ni wapi alitua ilikuwa ni lazima wajua ni mahali gani ndege ikiwa angani aliruka na kufungua parachuti.
Na kitendawili kingine kama ikitokea wakagundua ni mahali gani angani ambapo aliruka itawapasa kung'amua ni muda gani Cooper alitumia kuwa katika 'mdondoko huru' (free fall) kabla hajafungua parachuti! Kwasabu mda mrukaji anaotumia kuwa katika free fall kabla hajafungua parachuti 'inadetermine' mahali anapotua ardhini.

Kwahiyo baada ya FBI kurusha ndege kutoka uwanja wa Seattle kuelekea uwanja wa Rona. Kwa kuzingatia maelezo waliyoyapata kuwa ndege ilitikisika majira ya saa mbili dakika kumi na tatu hivyo basi FBI wakafikia muafaka kuwa huo ndio muda ambao Cooper alifungua mlango wa nyuma ya mkia wa ndege na kuruka! Kwahiyo FBI nao wakarusha maafisa kadhaa katika usawa ule ule wa anga na walibakia katika free fall tofauti tofauti kabla hawajafungua maparashuti! Baada ya maafisa wote kutua wakatafuta mzingo (circumference) wa eneo hilo ambalo ndio eneo pekee lililokuwa na uwezekano wa Cooper kutua siku aliporuka.
Na baada ya kubaini ili eneo ambalo Cooper alitua, walibaini pia kuwa siku ya tukio eneo hili lilikuwa na mvua kali na kimbunga! Hivyo basi ukizingatia kuwa Cooper aliruka ndege ikiwa umbali wa futi 10,000 kutoka ardhini na siku ilikuwa na mvua kubwa iliyoambatana na kimbu na pia ilikuwa ni usiku wa giza totoro wakakubaliana kuwa hakukuwa na uwezekano wa Cooper kutua akiwa hai.

Pia walizingatia sababu nyingine kuwa kumbuka siku ya tukio Cooper aliletewa maparavhuti ya kijeshi alafu akayakataa akadai apewe paruchuti nne za kawaida na FBI wakenda kwenye kituo cha kufundisha skydiving na wakampatia. Sasa kwenye yale maparachuti manne, mawili yalikuwa kwa ajili ya kufundishia tu darasani na mawili ndio yalikuwa hasa yanaweza kutumika kuruka angani.

Kitu cha ajabu ni kwamba FBI wlikuja kugundua kuwa Cooper aliyaacha yale maparachuti mawili ambayo ndio yanayopaswa kutumia kurukia na na akaruka na yale mawili ya kufundishia darsani ambapo parachuti moja walidhani kuwa alivaa yeye na lingine alifunga begi la fedha.
Kwahiyo kama ilivyoelezwa awali kuwa siku hiyo ilikuwa na mvua kubwa na kimbunga kwahiyo FBI waliamini kuwa maparachuti hayo ya kufundishia yasingeweza kuhimili hali ya hewa ya siku hiyo na kumuwezesha Cooper kutua salama, hivyo walifanya kazi wakiwa na hisia kuwa Cooper hakutua salama.

Baada ya kubaini eneo ambalo ndilo lilikuwa na uwezekano mkubwa wa Cooper kutua, eneo ambalo lilikuwa nyikani kuzunguka mto Lewis karibu na ziwa Merwin! FBI kwa kutumia maofisa waliokuwa kwa miguu ardhini na helicopters angani wakafanya kazi ya kulikagua eneo lote hilo.
Lakini pia FBI wakatumia ndege na helicopters kukagua njia inayopitwa na ndege kutoka Seattle kwenda Rona (vector 23). Baada ya msako na upekuzi wa eneo lote hilo kwa siku kadhaa FBI hawakufanikiwa kumpata Cooper hai au amekufa, hakupata hata mabaki ya vifaa vya parachuti wala mabegi.
Pia walitumia submarine kutafuta chini ya sakafu ya Mto Lewis na Ziwa Merwin lakini kote hakukuwa na dalili ya Cooper wala mabaki ya vifaa alivyoruka navyo.

Baada ya mwaka mzima 1971 kuisha pasipo mafanikio yoyote ya kumpata Cooper hai au mwili wake au hata mabaki ya vifaa alivyoruka navyo FBI ikabidi iombe msaada kutoka jeshi la marekani kusaidia msako huo. Hivyo basi jeshi la marekani wakatoa wanajeshi 200 kusaidia msako huo, pia wakapata msaada kutoka jeshi la Anga (Air force), pamoja na wanajeshi kutoka jeshi la ulinzi wa ndani ya nchi (national guard troops).
Kwa pamoja wakafanya msako wa kina zaidi katika eneo lote ambalo lilidhaniwa kuwa kuna uwezekano Cooper ndipo alipotua. Pia kampuni ya EEC ambayo inahusika na kufukua vitu vilivyozama majini (marine salvage firm), ilijitolea submarine ili kufanya msako chini ya ziwa Merwin kuona kama labda yeye Cooper au vitu alivyoruka navyo alizama humo.

Msako huu wa kina uliohusisha maafisa wa FBI, jeshi la marekani, makampuni binafsi pamoja na national guard troops ulifanyika kwa siku kumi na nane ndani ya mwezi march mwaka 1972 na pia ukafanyika tena mwezi April 1972 kwa siku kumi na nane nyingine.
Msako ulikuwa wa kina hasa kwani nukta baada ya nukta ilikaguliwa kwenye eneo lote ambalo walihisi cooper labda ametua ardhini na majini lakini mpaka msako huu unaisha ndani miezi miwili hiyo hawakufanikiwa kupata hata unywele au kipande cha nyuzi ya nguo ya Cooper au mabaki ya kitu chochote ambacho aliruka nacho siku ya tukio.

Kitendawili kikawa kigumu zaidi. Baada ya misako mingine mirefu zaidi bila mafanikio FBI ikawabidi waje na nadharia nyingine kwamba labda walikuwa wanafanya msako sehemu ambayo sio sahihi. Safari hii ikawabidi wafanye mahesabu ya kisayansi kabisa kwa kuzingatia kasi ya upepo siku ya tukio na uzito wa Cooper na mizigo aliyokuwa nayo na matokeo ya nadharia yao mpya ya mahesabu ya kisayansi ikawaambia Cooper atakuwa alidondokea eneo la kusini mashariki ya eneo walilokuwa wanafanya msako sasa. Eneo hili jipya walilolibaini kwa kuongozwa na hesabu za kisayansi lilikuwa linazunguka mto Washougul.
Hapa napo msako mkali ukafanyika kwa miezi kadhaa bila mafanikio yoyote.

Baada ya FBI kuona kuwa hakuna mafanikio yoyote katika misako yao ya maeneo ambayo walidhani labda Cooper alitua ikawabidi wabadilishe nadharia yote. Sasa wakaweka nadharia mpya kuwa labda kuna uwezekano Cooper alitua salama salimini na yuko mtaani anatumbua hela zake.
Hivyo basi kwa kuwa FBI walizipiga picha noti moja moja ya fedha zote alizopewa Cooper (kumbuka walimpa noti 10,000 za dola 20). Kwahiyo walikuwa na serial number ya kila noti aliyopewa Cooper. FBI wakasambaza serial number hizi kwenye mabenki, macasino, maduka na kila sehemu ambayo fedha inatumika lengo ni kuwa kama noti hata moja ambayo Cooper alipewa itatumiaka mahali popote na kuingia kwenye mzunguko wa hela basi FBI watadetect na kutrace hiyo hela imetoka kwa nani.

Lakini wakasubiri miezi na miaka hakuna noti hata moja ambayo iliingia kwenye mzunguko wa hela.
Kitendawili kikazidi kuwa kikubwa zaidi! Kama Cooper hakufanikiwa kutua salama kwanini wameshindwa kupata mwili wake au mabaki ya vitu alivyoruka navyo ukizingatia kuwa wamefanya msako nukta baada ya nukta ya sehemu ambayo alitua. Na kama alitua salama na kuingia mtaani, kwanini hazitumii hela alizozipata maana hakuna noti hata moja kwenye mzunguko.
Fumbo hili liliwatesa FBI kwa miaka saba mpaka mwaka 1978 ambapo mwanga kidogo ulipatikana kuhusu tukio hili..

VIDHIBITI VINAFANYA FUMBO KUWA GUMU ZAIDI BADALA YA KUSAIDIA
Mwaka 1978 muwindaji mmoja aliokota kikaratasi chenye maelekezo ya namna ya kushusha mlango wa nyuma wa ndege aina ya Boeing 737 (Northwest Orient Flight 305 ilikuwa ni Boeing 727) na FBI wanaamini labda kikaratasi hiki kilidondoshwa na Cooper.. Lakini kidhibiti hiki hakikusaidia sana.

Kidhibiti ambacho kilikuwa na mchango mkubwa kwenye kuleta maswali zaidi kwa FBI kilipatikana mwaka 1980.
Mtoto wa miaka 8 aliyeitwa Brian Igram akiwa kwenye vacation na familia yake kwenye beach ya mto Columbia alikuwa akichimba chini ili kusaidia familia kuwasha moto waote. Igram alikuwa akichimba kwa mikono kama watoto wafanyavyo na akachimba shimo refu kiasi na akiwa anachimba alikutana na makaratasi. Baada ya kuyatoa hayo makaratasi kutoka kwenye shimo alilochimba wazazi wake waligundua kuwa zilikuwa na vibunda vitatu vya hela.

Baada ya kuzichunguza kwa makini wazazi wakahisi kuwa inawezekana fedha hizo zinahusiana na D.B Cooper tukio ambalo lilitawala kwenye vyombo vya habari kwa kipindi hicho. Hivyo basi wazazi wakawasiliana na vyombo vya ulinzi na baada ya FBI kuzisoma serial number za noti hizo wakathibitisha kuwa ni kweli noti hizo ni sehemu ya fedha alizopewa D.B Cooper mwaka 1971. Swali, je zilifikaje pale?
Hivyo basi FBI ikatumia wataalamu wake ili kupata mwanga kidogo.
Kwanza vibunda vyenyewe vya hela vilikuwa kama ifuatavyo; kila kibunda kilikuwa peke yake kinajitegemea kimoja kilikuwa na noti 100 zilizofungwa pamoja kwa rubber band isipokuwa kibunda kimoja tu ambacho kikikuwa na noti 90 lakini nazo zilifungwa pamoja kwa rubber band.

Pia licha ya kuwa noti zilikuwa zimefungwa pamoja kwa rubber band lakini zilikuwa zimekaa hovyo hovyo katika umbo la mviringo na wataalamu wa FBI wakatoa conclusion kwamba zilikuwa zimekaa hovyo hivyo kwa umbo mviringo kwasababu zilikuwa zime 'kururuka' na maji ya mto kutoka mahali fulani na kuna kunasa hapo.
Na hakika huu ndio ufafanuzi ambao angalau ulikuwa unaingia akilini.
Lakini swali linakuja; inawezekanaje vibunda vitatu vya hela ambavyo havijaungana kila kimoja kinajitegemea 'vikururuke' na maji alafu vije vyote vinase sehemu moja? Kitu kama hicho ni almost imposible.
Kutokana na kesi hii kuteka vyombo vya habari kipindi hicho kugundulika kwa noti hizi kuliteka hisia za watu na hii ikapelekea mtaalamu wa jiolojia aliyeitwa Leonard Palmer kutoka chuo kikuu cha Portland kufanya tafiti katika beach ambayo vibunda hivi vitatu vilipatikana na matokeo ya utafiti wake ndio yalishangaza zaidi FBI.

Kwanza kabisa kumbukumbu zilionyesha kuwa sehemu kubwa ya mto Columbia ikiwemo sehemu vinunda hivi vya hela vilipatikana ilifanyiwa dredging mwaka 1974. Dredging ni vile wanatumia vifaa maalum kutoa udongo chini ya mto na pembezoni mwa mto na kuumwaga kwenye beach ya mto. Kitendo hiki huwa kinafanyika ili kuongeza kingo za mto au kuboresha ubora wa beach.
Sasa basi, alichokigundua huyu mtaalamu ni kwamba katika lile shimo ambalo mtoto Igram alichimba na kukuta vinunda vya hela za Cooper chini yake kulikuwa na matabaka mawili ya udongo na ukichimba tena unakutana na tabaka la tatu ambalo lina udongo wa mfinyanzi ambao ndio udongo unaopatikana baada ya kufanya dredging. Sasa hii ina maana gani? Maana yake ni kwamba hivyo vibunda vya hela za Cooper vilikuwa deposited hapo baada ya dredging kuwa imeshafanyika. Sasa kumbuka kuwa dredging ilifanyika mwaka 1974 na tukio la Cooper likitokea mwaka 1971.

Kuna tofauti ya miaka miatatu hapo. Sasa je hivi kweli inawezekana hela zikururuke na maji miaka mitatu na kwa bahati mbaya au nzuri isiyomithilika bibunda vitatu vyote vikwame sehemu moja?
Kama hiyo haitoshi; kumbuka kuwa mtaalamu anasema kuwa chini ya shimo alilochimba mtoto Igram kulikuwa na matabaka mawili ya udongo ndipo ufikie tabaka la udongo mfinyanzi uliotokana na dredging hii inamaanisha kuwa baada ya dredging kufanyika mwaka 1974 ilipita miaka kadhaa amabapo yale matabaka mawili mengine yakajitengeneza kwa juu ya udongo mfinyanzi ndio hivyo vibunda vya hela za Cooper zikawa deposited hapo.
Na mtaalmu alikisia hivyo vibunda vya hela vimekuwa deposited hapo labda miaka miwili tu iliyopita. Sasa huo ulikuwa ni mwaka 1980, miaka miwili nyuma maana yake ni 1978 na kumbuka tukio la Cooper lilitokea mwaka 1971.! Kuna tofauti ya miaka saba hapo katikati. Na hili lilikuja kuungwa mkono na kikosi kazi maalum kilichoundwa baadae na FBI kilichojulikana kama Cooper Research Team kuwa vibunda vya hela lazima vilikuwa deposited hapo miaka kadhaa baada ya tukio la sivyo rubber band walizozikuta vimeshikilia noti zingekuwa zimeharibika kabisa.

Ugunduzi huu uliwapa maswali na kuwachanganya zaidi FBI badala ya kuwasaidia kwasababu haiingii akilini hela zikururuke na maji miaka saba.
Kumbuka umbali kutoka mto Columbia na 'Vector 23' (njia ambayo ilipita ndege ya akina Cooper siku ya tukio) kulikuwa na umbali wa kilometa 20.
Hivyo basi hata kama maji yangekuwa yanatembea taratibu isingechukua zaidi ya dakika 40 kwa vibunda hivyo kufika hapo. Kwahiyo kwa namna yoyote ile isingewezekana kwa sehemu ya kuchukua dakika 40 itumike miaka saba, na kwa namna yeyote ile habadani haiwezekani vibunda vitatu ambavyo havijashikana vije vikwane exactly sehemj moja!
Katika ofisi ya FBI maswali na mafumbo yalikuwa mengi kuliko majibu! Hizo fedha za Cooper zimefikaje pale? Zimekuja na maji? Mtu kaziweka? Kama ni mtu kwanini aziweke pale? Je, fedha nyingine ziko wapi? Kwnini vibunda viwili vina noti 100 kila kimoja na kibunda kimoja kina noti 90 tu? Noti kumi zimeenda wapi? Na hii inatoa clue gani kuhusu D.B Cooper?

Baada ya miaka sita ya kitendawili kuhusu fedha zilizookotwa zimetoka wapi hatimaye mwaka 1986 FBI ikanyoosha mikono juu na kusalimu amri kuwa fedha hizo zilizookotwa haziwezi kuwasaidia kumpata Cooper. Hivyo basi wakafikia makubaliano ya kuziganya fedha. FBI wenyewe wakachukia noti 14 kama kidhibiti na noti zilizobaki zikagawanywa kwa kijana Igram aliyeziokota na nyingine wakapewa kampuni ya Bima waliowalipa fidia Northwest Orient Airlines.
Igram aliziuza kiasi kidogo cha baadhi ya noti zake mwaka 2008 katika mnada wa hadhara kwa thamani ya Dola 37,000.
Mpaka leo hii noti nyingine zilizobakia ambazo Cooper alipewa mwaka 1971 (takribani noti elfu tisa na mia saba) hazijulikani zilipo.

SAIKOLOJIA YA MKAKATI WA COOPER
Baada ya miaka mingi ya upelelezi na kujiuliza maswali mengi hatimae mwaka 2007 FBI walitangaza kwa umma baadhi ya mambo waliyoyabaini katika mkasa mzima wa D.B Cooper.
Kwa mfano siku ya tukio Cooper alihitaji parashuti moja tu ili aweze kuruka lakini aliwaagiza kuwa anahitaji maparashuti manne. FBI wanaamini kuwa Cooper alitoa maagizo ya dizaini hii ili kupandikiza wazo kwa vichwani mwa maofisa wa FBI kuwa kulikuwa na uwezekano akaruka na mateka ambao watatumia maparashuti mengine matatu yaliyobaki. Hii iliwalazimu FBI kumpatia maparashuti manne ambayo hayana hitilafu au ubovu wowote. Na iliwachukua muda sana kubaini kuwa Cooper alicheza na akili zao bila wao kujua.
Pia uchaguzi wa kuiteka Northwest Orient Flight 305 haukuwa wa bahati mbaya. FBI wanaamini kuwa Cooper alifanya uchunguzi wa kina na kuchagua kuiteka ndege hiyo. Kumbuka kuwa Orient Flight 305 ilikuwa ni aina ya ndege ya Boeing 727.

Kwa kipindi hicho Boeing 727 ndio zilikuwa ndege pekee ambazo zilikuwa na uwezo wa kufunguliwa mlango wa nyuma mkiani ikiwa bado iko angani. Kitu hiki kilikuwa hakijulikani kwa raia na hata watu wa ndege wenyewe walikuwa hawafahamu jambo hili.
Na taarifa hii ilifichwa kwasababu kwa kipindi hiki haikuwa kitu cha kawaida kwa ndege ya abiria kuwa na ubunifu wa aina hii.
Watu pekee ambao walikuwa wanafahamu suala hili na kuwahi kutumia advantage ya ubunifu huu walikuwa ni CIA ambao walitumia ndege kama hii kudondosha mizigo na maafisa wao katika maeneo husika katika vita ya Vietnam.

Pia injini za Boeing 727 zilikuwa juu kidogo tofauti na ndege nyingine za abiria ambazo injini zake zilikuwa chini chini karibia usawa wa madirisha. Kumbuka kuwa injini ya ndege ikiwashwa ikiwa inazunguka kitu chochote kikipita mbele yake kinavutwa na kumezwa kwenye injini na kuharibiwa au injini yenyewe kupata hitilafu. Hivyo basi uchaguzi wa kuruka kutoka kwenye Boeing 727 ilimaanisha kuwa ilipunguza hatari ya mrukaji kuvutwa na kumezwa na injini.
Pia FBI wanaamini kuwa Cooper alifahamu kuwa Boeing 727 ilikuwa na teknolojia mpya ambayo iliruhusu kujaza mafuta kwenye matanki matatu ya ndege kwa kutumia tundu moja tu. Kama isingekuwa na teknolojia hiyo hiyo ya kujaza mafuta kwa tundu moja tu FBI wangeweza kutumia mwanya wa gari la kujazia mafuta likiwa linazunguka upande mwingine wa ndege kupenyeza maafisa wao.

Pia Boeing 727 ilitoa advantage nyingine katika ufunguaji wa mlango wa nyuma wa ya mkia wa ndege ambapo ukiwasha tu kifaa cha kufungua mlango huo hata rubani aliye mbele hawezi kuufunga. FBI wanaamini Cooper alilifahamu hili ndio maana baada ya kuwafungia watu aliobaki nao kwenye chumba cha rubani. Alifungua mlango wa nyuma kwa kujiamini na kuruka.
Pia Boeing 727 ilikuwa na ubunifu mwingine adhimu tofauti na ndege nyingine kwa kuwa ilikuwa unaweza kucontrol speed na mwinuko wa ndege 'manually' hata ukiwa katika sehemu ya kukaa abiria, pia kwa kipindi hicho Boeing 727 ndio ilikuwa ndege pekee ya abiria ambayo ilikuwa na uwezo wa kugeuza mabawa yake ili yakae katika nyuzi 15.

FBI wanaamini kuwa Cooper alifanya utafiti wa kina na kuweka mkakati kabambe kabla ya kutekeleza tukio na alitumia advantage zote hizi za ndege ya Boeing 727 ili kutekeleza tukio lake kwa ukamilifu wa 100%.
Lakini jambo lingine la muhimu zaidi ilikuwa ni uchaguzi wa siku ya tukio. November 24.
Kwanini? Baada ya tukio FBI kugundua Cooper alikuwa ameruka nyikani wazo mojawapo ambalo walilipata ni kwamba kwakuwa sehemu aliyoruka ilikuwa mbali mno na makazi ya watu, hivyo basi ingemchukua Cooper takribani siku hata tatu kusafriri ili kurudi mtaani.

Kwahiyo FBI walidhani kwa kuwa Cooper asingeliwezakutumia siku moja kusafiri kurudi mtaani hivyo basi kama kesho yake wangembelea kila ofisi na maeneo ya kazi kukusanya orodha ya watu ambao hawajatokea kazini lazima watu hao mmoja wao angekuwa ni Cooper.
Lakini hii ilikuwa haiwezekani! Kwanini? Kwasababu November 24 usiku wake ulikuwa ni sikukuu ya 'Thanks giving' maana yake ni kwamba kesho yake haikuwa siku ya kazi. Mbaya zaidi November 24, 1971 ilikuwa ni siku ya Jumatano kwahiyo kesho yake alhamisi pamoja na ijumaa zilikuwa siku za sikuu na siku zilizofuata zilikuwa ni weekend. Kwahiyo hii ilimpa Cooper siku nne za kutosha kabisa kusafiri kutoka nyikani mpaka mtaani. Na kama alikuwa mfanyakazi ofisi fulani maana yake Jumatatu aliingia ofisini kama watu wengine! FBI wakapiga saluti.

MAISHA BAADA YA TUKIO LA D.B COPPER
Baada ya tukio la utekaji la Cooper kutokea na FBI kuonekana dhahiri kuwa wameshindwa kufikia mwisho wa kutengua kitendawili cha tukio hili hali ilikuwa tete katika viwanja vya ndege na kusababisha marekebisho mengi ya protokali za ulinzi na utoaji huduma katika viwanja vya ndege nchini marekani.
Kwanza kabisa serikali ya marekani ilitilia mkazo uanzishwaji upya na kuboresha programu ya maaskari wanaosindikiza ndege za abiria (Sky Marshal Program).
Pia serikali ilichukua hatua kali zaidi kwa mara ya kwanza kabisa kuanzisha mpango wa kupekua mizigo ya abiria kabla hawajapanda kwenye ndege. Hatua hii ilisababisha mvutano mkali kati ya wananchi wa marekani na serikali yao katika miaka ya sabini ambapo ilifikia hatua kesi za kikatiba zilifunguliwa dhidi ya serikali ya marekani kwa madai ya kwamba kupekua mizigo ya abiria ilikuwa inavunja Kipengele/Marekebisho ya Nne ya katiba ya marekani (Fourth Amendment) kipengele kinachomlinda raia wa marekani dhidi ya upekuzi na kuingiliwa faragha yake. Lakini mwishoni serikali ilishinda kesi hizi na tangu hapo imekuwa ni jambo la lazima kwa mizigo kukaguliwa kabla ya abiria kupanda ndege.

Si hivyo tu, serikaki kupitoa idara ya usafiri wa anga nchini marekani (FAA) ikaenda mbali zaidi kwa kuzitaka kampuni zote za usafiri wa anga zinazotumia ndege aina ya Boeing 727 wafunge kifaa maalum cha kuzuia mlango wa nyuma mkiani mwa ndege kufunguka pindi ndege ikiwa angani. Kifaa hiki kilipewa jina 'Cooper Vane'.
Na pia FAA walitoa maagizo kuwa ndege zote ziwekwe matundu maalum ya kuchungulia (peepholes) katika mlango wa chumba cha marubani ili kuwawezesha waweze kuona kinachoendelea upande wa abiria.
Pia, mwaka 2013 Earl Cossey mmliki wa kituo cha kufundisha Skydiving sehemu ambapo maparashuti manne yaliazimwa na FBI na kumpa Cooper mwaka 1971 alikutwa ameuawa nyumbani kwake. Bw. Cossey alikuwa ameajiriwa na FBI mara tu baada ya tukio la Cooper akiwa kama mshauri muelekezi (consultant) katika juhudi za kumtafuta Cooper na alihusika katika hatua zote za upelelezi.

Ziko nadharia nyingi zinazoamini kuwa vyombo vya usalama vya marekani vinahusika katika kifo cha Cossey na watu wanadhani kuwa kuna jambo la siri ambalo alikuja kulibaini katika upelelezi huo wa tukio la Cooper na FBI walihofia labda Bw. Cossey asingeliweza kutunza siri hiyo, hivyo basi suluhisho jepesi wakaona ni kumwondosha.
Hatimaye..
Mwezi July mwaka huu 2016 tarehe 14, shirika la upelelezi la FBI walifunga jalada la kesi ya Cooper na kukivunja kikosi kazi maalum cha kuchunguza tukio la Cooper (Cooper Research Team) kwa madai kuwa haukukuwa na tumaini lolote la kufikia hitimisho katika upelelezi huo.
Walifunga jalada wakiwa bado hawafahamu kama Cooper yuko hai au ameshafariki, hawajui kama hilo ni jina lake halisi au la kubuni, hawafahamu fedha alizopewa zimekwenda wapi na wala hawafahamu ni namna gani binadamu mmoja alifanikiwa kutekeleza tukio kwa usahihi wa asilimia mia moja kama tukio hili.

Tukio la Utekaji la Cooper ndilo limeingia kwenye orodha ya kumbukumbu ya shirika la FBI kama kesi iliyotumia muda mrefu zaidi kufanyiwa uchunguzi (miaka 45) na tukio hili limeingia kwenye vitabu vya historia ya nchi ya marekani kama tukio pekee la utekaji wa anga (hijacking) ambalo limeshindikana kufikia hitimisho.
Kwa hivi sasa katika maeneo mbalimbali nchini marekani na hasa eneo la Airel, mjini Washington kila mwaka mwezi November watu husherehekea 'Cooper day' kukumbuka tukio hilo la kihistoria nchini marekani lilotekelezwa na binadamu mmoja peke yake ambaye kutokana na ustadi alioutumia kufanikisha azma yake amebakia kwenye vitabu vya historia, na umahiri wake umemfanya kugeuzwa kutoka kuwa binadamu wa kawaida mpaka kuwa 'binadamu wa kusadikika'! Mwenyewe alijitambulisha kama D.B Cooper!

Mwisho.